Sifa za Kuchaguliwa Kidato cha Tano 2025

 0
Sifa za Kuchaguliwa Kidato cha Tano 2025

Vigezo vya Kuchaguliwa Kidato cha Tano 2025/2026

Baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutangaza matokeo ya Kidato cha Nne tarehe 23 Januari 2025, wahitimu pamoja na wazazi wao wanajikita zaidi katika kufahamu kama wamekidhi vigezo vya kujiunga na Kidato cha Tano. Shule za sekondari za serikali zinaendelea kuwa chaguo la wengi kutokana na gharama nafuu na ubora wa elimu zinazotoa.

Hata hivyo, kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule za serikali si jambo rahisi, kwani kuna vigezo mahususi vinavyotakiwa kutimizwa. Ili kusaidia wanafunzi na wazazi kufahamu taratibu za uchaguzi, hapa tunakuletea muhtasari wa sifa na masharti ya kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2025/2026.


1. Vigezo Muhimu vya Kuchaguliwa Kidato cha Tano

i. Ufaulu wa Masomo

  • Mwanafunzi anatakiwa awe na ufaulu wa masomo yasiyopungua matatu (3) kwa daraja la "Credit" (yaani A, B, au C).
  • Masomo ya dini hayahesabiwi katika kigezo hiki.

ii. Jumla ya Alama za Ufaulu

  • Jumla ya alama katika masomo saba (7) aliyopewa daraja hazipaswi kuzidi alama 25.
  • Kigezo hiki kinawapendelea wanafunzi waliofanya vizuri kwa ujumla katika mitihani yao.

iii. Alama za Tahasusi

  • Wanafunzi wanapaswa kuwa na jumla ya alama kati ya 3 hadi 10 katika masomo yao ya tahasusi.
  • Hairuhusiwi kuwa na alama "F" katika somo lolote la tahasusi.

iv. Umri wa Mwanafunzi

  • Mwanafunzi hapaswi kuwa na umri wa zaidi ya miaka 25 wakati wa udahili.

v. Ushindani na Upatikanaji wa Nafasi

  • Uchaguzi wa wanafunzi utafanyika kwa misingi ya ushindani, kulingana na nafasi zilizopo katika shule mbalimbali.
  • Hata kama mwanafunzi amekidhi vigezo vyote, bado anaweza asichaguliwe ikiwa ushindani ni mkubwa na nafasi ni chache.

vi. Sifa Linganishi kwa Wanafunzi wa Mifumo Mingine ya Elimu

  • Wanafunzi waliofanya mitihani kutoka mifumo mingine ya elimu nje ya NECTA watahitajika kuomba udahili kupitia matokeo yaliyofanyiwa ulinganifu na Baraza la Mitihani Tanzania.

2. Mambo Muhimu ya Kuzingatia

Fuatilia matokeo yako kwa umakini ili kujua kama unakidhi vigezo vya kuchaguliwa.
Angalia shule zinazopokea wanafunzi kwa mchepuo unaotaka kusomea ili uweze kupanga mipango yako mapema.
Wasiliana na Wizara ya Elimu au Baraza la Mitihani kwa taarifa rasmi kuhusu taratibu za udahili na maelekezo ya usajili.

Kwa taarifa zaidi, unaweza kutembelea tovuti ya Wizara ya Elimu (www.moe.go.tz) au Baraza la Mitihani Tanzania (www.necta.go.tz).