Jinsi ya Kurekebisha Taarifa kwenye Kitambulisho cha Taifa (NIDA)
Jinsi ya Kurekebisha Taarifa kwenye Kitambulisho cha Taifa (NIDA)

Mwongozo wa Marekebisho ya Taarifa za Usajili na Utambuzi wa Watu umeainisha sifa stahiki, aina ya taarifa zinazoruhusiwa kurekebishwa na vigezo hitajika kuwasilishwa na mwombaji kwenye ofisi ya Usajili wilayani ili ombi liwe na sifa ya kuanza kufanyiwa kazi:-
Sifa Stahiki kwa Mwombaji Mwenye Hitaji la Kuboresha Taarifa za Usajili: -
(i) Mwombaji aliyeolewa na kubadilisha jina kwa kutumia taarifa za ukoo wa mume/mwenza wake,
(ii) Mwombaji aliyeolewa na kuachika kisheria anaweza kuruhusiwa kubadilisha taarifa zake na kurudia kujiandikisha kwa majina yake ya awali ya kabla hajaolewa kulingana na vyeti/nyaraka zake
(iii) Mwombaji aliyekosea kuandika baadhi ya taarifa zake yeye mwenyewe ambazo aliziandikisha wakati wa zoezi la Usajili na Utambuzi.
(iv) Mwombaji ambaye taarifa zake hazikuingizwa kwa usahihi kwenye mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na Watendaji wake wakati wa utekelezaji wa majukumu husika (Operational issues),
(v) Mwombaji ambaye aliandikisha taarifa/majina yake yoyote kwenye kipengele cha majina mengine/maarufu na baadaye akahitaji majina yake hayo yaandikwe kwenye kipengele cha majina ya kwanza basi ataweza kurekebishiwa bila kuathiri utambulisho wake wa awali au taarifa zilizohifadhiwa katika mfumo.
(vi) Jina la ukoo iwapo mwombaji ataamua kutumia jina ambalo tayari lipo kwenye upande wa majina ya wazazi wake mfano jina la Babu ambalo hapo awali hakulitumia.
Afisa Usajili wa Wilaya (DRO) anaweza akaridhia kubadilisha taarifa ambazo ziko kwenye fomu ya maombi ya Mwombaji ambazo ziliandikishwa hapo awali mfano katika sehemu ya majina mengineyo na iwapo mabadiliko hayo hayana nia ovu au yenye lengo la kuficha Utambulisho wake wa awali.
Taarifa za Maombi ya Utambulisho wa Watu zinazoruhusiwa kubadilishwa
Mwongozo wa marekebisho ya Taarifa za Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa unaelekeza juu ya taarifa zinazoruhusiwa kubadilishwa iwapo m waombaji kakidhi vigezo vya msingi vinavyo hitajika ni pamoja na; -
(i) Jina la kwanza, la kati, au la Mwisho (Ukoo) baada ya kukidhi vigezo na kuwasilisha uthibitisho unaotakiwa,
(ii) Tarehe na mwezi wa kuzaliwa,
(iii) Makazi ya mwombaji,
(iv) Namba ya simu baada ya Afisa Usajili kujiridhisha ya kwamba Namba ya Simu imesajiliwa kwa kutumia NIN ya Mwombaji.
(v) Uraia kwa yule aliyebadilisha uraia kwa nyaraka zinazokubalika kwa kufuata mwongozo wa Uhuishaji wa Taarifa za Uraia
(vi) Taarifa ya ndoa,
(vii) Taarifa ya kazi pamoja na
(viii) Kumbukumbu binafsi (taarifa hizi zinapatikana kwenye kipengele F cha fomu ya Usajili na Utambuzi wa Watu Na. 47- 58.)
Taarifa za Mwombaji zisizoruhusiwa kubadilishwa isipokuwa kwa kibali maalumu baada ya kufanyiwa kazi na Kamati ya Usajili na Utambuzi na kupata idhini ya Mkurugenzi Mkuu
(i) Taarifa za Wazazi
(ii) Makazi ya Kudumu
(iii) Mahali pa kuzaliwa
(iv) Majina mawili/ matatu
(v) Mwaka wa kuzaliwa na
(vi) Saini ya mwombaji
Taratibu mbalimbali za kufanya marekebisho ya taarifa kutokana na aina ya taarifa au usajili:
Mabadiliko ya Majina
Mwombaji yoyote anayehitaji kufanya mabadiliko ya majina anahitajika kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
Mabadiliko ya Majina
a) Kadi ya kliniki, tangazo, cheti cha kuzaliwa, cheti cha darasa la vii, kidato cha iv ama ‘leaving certificate’ vilivyotafutwa na wazazi awali au ulivyo viwasilisha NIDA wakati unasajiliwa na vimebeba taarifa za jina la unavyohitaji lisomeke kwa sasa,
b) Kata hati ya kiapo cha kubadili jina (Deedpoll) toka kwa wakili anayetambuliwa na Chama cha Mawakili Tanzani (TLS) kisha kiwasilishe Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata Usajili wa Jina unalorekebisha,
c) Toa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali linalotolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuonyesha mabadiliko ya jina yaliyofanyika,
d) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka zozote zaidi ambazo ataona zinafaa kuthibitisha taarifa/majina ya mwombaji husika,
e) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kuyafanyiwa kazi na watendaji wote,
f) Iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote lah utapaswa kulipia shilingi 20,000/=,
g) Ombi la mteja litawasilishwa kwenye kamati ya Usajili na Utambuzi wa watu, iwapo watajiridhisha kuwa ombi limekidhi vigezo ndipo watatoa kibali ili Afisa Msajili aweze kuendelea na hatua ya kufanya maboresho, ombi lisipokidhi vigezo, kibali hakitatolewa na Afisa Msajili haruhusiwi kuendelea na hatua yoyote ya maboresho.
Taarifa za Maombi ya Utambulisho wa Watu zinazoruhusiwa kubadilishwa
Mwongozo wa marekebisho ya Taarifa za Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa unaelekeza juu ya taarifa zinazoruhusiwa kubadilishwa iwapo m waombaji kakidhi vigezo vya msingi vinavyo hitajika ni pamoja na; -
a) Cheti cha ndoa (Marriage certificate) cha Serikali,
b) Cheti cha talaka (Divorce certificate) cha Serikali au Nakala ya hukumu (Judment/Decree) au nyaraka ya kukaza hukumu,
c) Cheti cha kuzaliwa au Vyeti vya shule ya Msingi/Sekondari/Elimu ya juu au Cheti cha ubatizo/falaki,
d) Afisa Usajili Wilaya ili kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anaweza akaomba nyaraka nyinginezo zozote zenye kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji husika,
e) Mwombaji anapaswa kuchangia gharama ya kubadili taarifa husika shilingi 20,000/= na iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote,
f) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka zozote zaidi ambazo ataona zinafaa kuthibitisha taarifa/majina ya mwombaji husika,
g) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kufanyiwa kazi na Maafisa Usajili wilaya.
Muhimu: - ombi la mteja linaweza kuafikiwa ama lah kutegemea na sababu na nia ya mteja kutaka kufanya maboresho ya taarifa zake
-------------------------------------------------------
Marekebisho ya Tarehe au Mwezi au Mwaka wa kuzaliwa
Mwombaji yoyote anayehitaji kufanya mabadiliko ya tarehe au mwezi au mwaka wa kuzaliwa anahitajika kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
Mabadiliko ya Taarifa ya Tarehe na Mwezi wa Kuzaliwa
a) Cheti cha kuzaliwa,
b) Ikiwa Mwombaji tayari alishawasilisha cheti chake cha kuzaliwa hapo awali wakati anasajiliwa na kuja kuwawasilisha cheti kingine kipya cha kuzaliwa chenye utofauti wa taarifa; Afisa Usajili husika anaweza kuomba uthibitisho wa nyaraka hiyo toka kwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (The Zanzibar Civil Status Registration Agency-ZCSRA),
c) Mwombaji aambatanishe na nakala ya Tangazo kutoka katika Gazeti la Serikali lenye taarifa za mabadiliko husika,
d) Afisa Usajili Wilaya ili kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anaweza akaomba nyaraka nyinginezo zozote zenye kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji husika,
e) Mwombaji anapaswa kuchangia gharama ya kubadili taarifa husika shilingi 20,000/=, na iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote,
f) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kufanyiwa kazi na Maafisa Usajili wilaya.
Mabadiliko ya Mwaka wa Kuzaliwa
Maombi ya mabadiliko ya Mwaka wa Kuzaliwa hayatoruhusiwa isipokuwa yamepata kibali maalum kutoka kwenye Kamati ya Usajili na Utambuzi. Aidha, Mwombaji atatakiwa kuonyesha nyaraka zifuatazo; -
a) Cheti cha kuzaliwa kilichopatikana kipindi cha awali kilichotafutwa na Wazazi/Walezi,
b) Cheti cha kumaliza Shule ya Msingi,
c) Kadi ya Kliniki (CLINIC),
d) Cheti cha kumaliza shule za sekondari (Leaving Certificate),
e) Nyaraka yoyote ya awali yenye uthibitisho wa miaka ya mwombaji iliyopatikana kabla ya Kusajiliwa na Kutambuliwa na kupata Kitambulisho cha Taifa,
f) Mwombaji aambatanishe nakala ya Tangazo kutoka katika Gazeti la Serikali lenye taarifa za mabadiliko husika,
g) Afisa Usajili Wilaya ili kutekeleza majukumu yake kwa usahihi anaweza akaomba nyaraka nyinginezo zozote zenye kuthibitisha taarifa/tarehe ya Mwombaji husika,
h) Mwombaji anapaswa kuchangia gharama ya kubadili taarifa husika shilingi 20,000/= na iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo kulazimika kulipia gharama yoyote,
i) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kufanyiwa kazi ngazi ya awali na Maafisa Usajili wilaya kabla ya kuwasilishwa kwenye Kamati husika kwa Maamuzi.
Muhimu: - ombi la mteja linaweza kuafikiwa ama lah kutegemea na sababu na nia ya mteja kutaka kufanya maboresho ya taarifa zake
Mabadiliko ya Taarifa za Makazi anayoishi Mwombaji
Mwombaji yoyote anayehitaji kufanya mabadiliko ya taarifa za makazi anahitajika kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
a) Barua kutoka Serikali ya Mtaa/Kijiji/Sheia anapoishi sasa na
b) Barua kutoka Serikali ya Mtaa/Kijiji alipokuwa anaishi kabla ya kuhamia kwenye Makazi mapya,
c) Aidha, katika kushughulika maombi ya marekebisho ya taarifa, Afisa Usajili anaweza akaomba nyaraka nyingine zozote zenye kuthibitisha taarifa ya Mwombaji, ambazo zinaweza zikamsaidia katika kutekeleza maamuzi yake kwa usahihi.
Muhimu: - ombi la mteja linaweza kuafikiwa ama lah kutegemea na sababu na nia ya mteja kutaka kufanya maboresho ya taarifa zake
Mabadiliko ya Taarifa Kundi la watumishi wa umma/watumishi wa umma waliostaafu
Taarifa za Mtumishi wa umma ambazo zinaweza kurekebishwa ni zile ambazo hazitaathiri utambulisho wake wa hapo awali na zitazingatia mambo yafuatayo; -
(i) Makosa yaliyofanywa na Watendaji wa Mamlaka katika utendaji wao wa kazi hususan kwenye marekebisho ya herufi,
(ii) Majina ambayo yameandikwa katika mpangilio wa tofauti (vice versa) na yote yapo katika sehemu ya majina husika,
(iii) Majina ya Mwombaji ambaye alijiandikisha kwa kutumia majina ya mwenza wake baada ya kuolewa na kwa kutoa uthibitisho wa cheti cha ndoa,
Mabadiliko ya Umri kwa kundi la watumishi wa umma/watumishi wa Umma waliostaafu
a) Barua ya utambulisho kutoka kwa Mwajiri wa Mwombaji ikithibitisha taarifa za maombi husika,
b) Kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma akiridhia mabadiliko husika,
c) Cheti cha kuzaliwa cha mwombaji chenye taarifa ya taarifa hijajika,
d) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka zozote zaidi ambazo ataona zinafaa kuthibitisha taarifa/majina ya mwombaji husika,
e) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kuyafanyiwa kazi na watendaji wote,
f) Iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo mwombaji kulazimika kulipia gharama yoyote lah utapaswa kulipia shilingi 20,000/=,
g) Ombi la mteja litawasilishwa kwenye kamati ya Usajili na Utambuzi wa watu, iwapo watajiridhisha kuwa ombi limekidhi vigezo ndipo watatoa kibali ili Afisa Msajili aweze kuendelea na hatua ya kufanya maboresho, ombi lisipokidhi vigezo, kibali hakitatolewa na Afisa Msajili haruhusiwi kuendelea na hatua yoyote ya maboresho.
Mabadiliko Majina kwa kundi la watumishi wa umma/watumishi wa umma waliostaafu
a) Barua ya utambulisho kutoka kwa Mwajiri wa Mwombaji ikithibitisha maombi ya kubailisha taarifa za maombi husika,
b) Kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma akiridhia mabadiliko husika,
c) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka nyingine yoyote atakayoona inafaa kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji.
d) Kata hati ya kiapo cha kubadili jina (Deedpoll) toka kwa wakili anayetambuliwa na Chama cha Mawakili Tanzani (TLS) kisha kiwasilishe Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata Usajili wa Jina unalorekebisha kisha ambatanisha kwa pamoja na risiti ya malipo husika,
e) Toa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali linalotolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuonyesha mabadiliko ya jina yaliyofanyika,
f) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kuyafanyiwa kazi na watendaji wote,
g) Iwapo makosa yamefanyika upande wetu, Afisa Usajili atajiridhisha na kuendelea na maboresho pasipo mwombaji kulazimika kulipia gharama yoyote lah utapaswa kulipia shilingi 20,000/=,
h) Ombi la mteja litawasilishwa kwenye kamati ya Usajili na Utambuzi wa watu, iwapo watajiridhisha kuwa ombi limekidhi vigezo ndipo watatoa kibali ili Afisa Msajili aweze kuendelea na hatua ya kufanya maboresho, ombi lisipokidhi vigezo, kibali hakitatolewa na Afisa Msajili haruhusiwi kuendelea na hatua yoyote ya maboresho,
Mabadiliko ya Majina Kutokana na Kuolewa au Kuachika kwa kundi la watumishi wa umma/watumishi wa umma waliostaafu
a) Barua ya utambulisho kutoka kwa Mwajiri wa Mwombaji ambayo inathibitisha taarifa za maombi husika,
b) Kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma akiwa amekubaliana na kuriridhia mabadiliko husika,
c) Cheti cha Ndoa/Talaka,
d) Kata hati ya kiapo cha kubadili jina (Deedpoll) toka kwa wakili anayetambuliwa na Chama cha Mawakili Tanzani (TLS) kisha kiwasilishe Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata Usajili wa Jina unalorekebisha kisha ambatanisha kwa pamoja na risiti ya malipo husika,
e) Toa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali linalotolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuonyesha mabadiliko ya jina yaliyofanyika,
f) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kuyafanyiwa kazi na watendaji wote,
g) Mwombaji analazimika kulipia shilingi 20,000/= ikiwa ni gharama ya marekebisho ya taarifa,
h) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka nyingine yoyote atakayoona inafaa kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji.
Mabadiliko kwa Wafanyakazi wa Serikali wasiotumia Mfumo wa Malipo wa Utumishi unaotumia Namba Maalumu ya Malipo ya Mshahara (Cheque Number) kwa Watumishi wa Umma
Inahusisha wafanyakazi wa Serikali wasio katika Payrol System kama vile Wanajeshi, Polisi na Taasisi zingine, Utaratibu wa kufuata ni pamoja na kuwasilisha kwenye ofisi ya Usajili ya NIDA wilayani; -
(i) Barua ya Utambulisho kutoka kwa Mwajiri wa mwombaji,
(ii) Kibali kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara husika kinachotoa idhini ya mabadiliko ya taarifa kufanyika,
(iii) Cheti cha kuzaliwa kwa mabadiliko ya majina na tarehe ya kuzaliwa,
(iv) Kata hati ya kiapo cha kubadili jina (Deedpoll) toka kwa wakili anayetambuliwa na Chama cha Mawakili Tanzani (TLS) kisha kiwasilishe Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata Usajili wa Jina unalorekebisha kisha ambatanisha kwa pamoja na risiti ya malipo husika,
(v) Toa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali linalotolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuonyesha mabadiliko ya jina yaliyofanyika,
(vi) Mabadiliko yoyote ambayo hayana ushahidi wa nyaraka sahihi katika kuthibitisha maombi ya taarifa husika hayawezi kuruhusiwa/kupokelewa au kuyafanyiwa kazi na watendaji wote,
(vii) Mwombaji analazimika kulipia shilingi 20,000/= ikiwa ni gharama ya marekebisho ya taarifa,
(viii) Afisa Usajili Wilaya anaweza akaomba nyaraka nyingine yoyote atakayoona inafaa kuthibitisha taarifa/majina ya Mwombaji,
Mabadiliko ya Taarifa kwa waombaji waliofanya udanganyifu wa taarifa
Waombaji hawa ni wale waliowasilisha nyaraka za kughushi au za watu wengine ili kuficha utambulisho wao halisi. Udanganyifu huu, ni ule uliofanyika awali katika usajili na utambuzi
Sheria ya Usajili na Utambuzi ya mwaka 1986 na marejeo ya mwaka 2012 na Kanuni zake za mwaka 2014 kifungu Namba (17) (b) kinaeleza kuwa:
Any person who: “knowingly gives false or misleading information to a registration officer;” commits an Offense and once convicted the person is liable to a fine of not less than two hundred thousand shillings and not more than five million shillings or to imprisonment for a term not less than two months and not more than two years”.
Mtu yeyote ambaye: "Kwa kujua anatoa taarifa za uongo au za kupotosha kwa Afisa Usajili; anatenda kosa na mara baada ya kupatikana na hatia mtu anawajibika kwa faini isiyopungua shilingi laki mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua miezi miwili na kisichozidi miaka miwili”
Mwombaji aliyethibitika kufanya udanganyifu, Mamlaka itafanya marekebisho baada ya kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
(i) Nakala ya hukumu/decree order,
(ii) Mwenendo wa kesi,
(iii) Nakala ya malipo ya faini kama atakuwa amehukumiwa hivyo,
(iv) Maelezo ya kukamilika kwa kifungo kama alifungwa,
(v) Nyaraka nyingine kama zilivyo ainishwa katika vipengele vilivyotangulia.
Mabadiliko ya taarifa kwa wageni wakazi/wakimbizi
Mwombaji ambaye sio raia wa Tanzania na ambaye anahitaji kubadilisha taarifa zake alizowasilisha wakati wa Utambuzi na Usajili atatakiwa kufanya mambo yafuatayo; -
(i) Kuwasilisha hati ya kusafiria,
(ii) Hati ya Mkazi halali ,
(iii) Barua ya Serikali ya Mitaa/Vijiji/Sheia aliokuwa anaishi na anakohamia kwa mabadiliko ya makazi,
(iv) Hati za utegemezi kwa wategemezi,
(v) Kiambata kinachoonyesha taarifa husika kama zilivyoandikishwa na Mamlaka za nchi anayotokea,
(vi) Nyaraka mpya inayoonyesha mabadiliko yanayotakiwa kufanyika,
(vii) Nyaraka zingine kutegemeana na kundi lake kama Mkimbizi au Mlowezi,
(viii) Kwa Wakimbizi atawasilisha nyaraka za Ukimbizi zinazotambuliwa na Idara ya Wakimbizi,
(ix) UNHCR Pamoja na barua kutoka Idara ya Wakimbizi ikiidhinisha mabadiliko husika ya taarifa zake,
(x) Kwa Walowezi; atawasilisha nyaraka za Ulowezi zinazotambuliwa na Idara ya Uhamiaji pamoja na barua kutoka ofisi hiyo ikiiridhia mabadiliko husika ya taarifa zake,
(xi) Risiti ya malipo kwa ajili ya huduma husika,
(xii) Nyaraka zingine zozote ambazo Afisa Usajili wa Wilaya atakavyoona inafaa kwa ajili ya kujiridhisha na maombi husika (Usahihi wa taarifa husika).