Nafasi za kazi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) - Machi 2025
Nafasi za kazi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) - Machi 2025

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
ISO 9001:2015 CERTIFIED
TAARIFA KWA UMMA
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya Mwaka 2003. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ina jukumu la kusimamia na kudhibiti Sekta ya Mawasiliano inayojumuisha Utangazaji, Posta, Simu na Intaneti.
Kwa masuala ya utangazaji, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa upande wa Tanzania Bara tu. Kifungu cha 26 (2) cha Sheria ya TCRA Na. 12 ya mwaka 2003 kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Utangazaji uwezo wa kuteua Wajumbe wa Kamati ya Maudhui. Kamati inatakiwa kuwa na Wajumbe wasiozidi watano akiwemo Mjumbe mmoja wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA ambaye atakuwa ni Mwenyekiti na Wajumbe wengine wanne
(4) huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Utangazaji kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA. Wajumbe wa Kamati ya Maudhui hawatakiwi kuwa waajiriwa wa TCRA au mashirika ya Utangazaji.
Maombi ya nafasi moja (1) yanakaribishwa kwa Mtanzania yeyote mwenye sifa na ujuzi stahiki wa kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maudhui.
SIFA ZA MWOMBAJI
Ili aweze kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maudhui, muombaji lazima awe na sifa zifuatazo:
(a) Awe mhitimu wa elimu ya Chuo Kikuu kinachotambulika;
(b) Awe mzoefu angalau wa miaka kumi katika moja au zaidi kwenye Usimamizi, Sheria, Uchumi, Fedha, Uhandisi, Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari, Utangazaji, Mawasiliano au Utamaduni;
(c) Awe na elimu/ujuzi katika Sekta ya Utangazaji;
(d) Kutimiza matakwa ya kutokuwa na mgongano wa kimaslahi chini ya kifungu cha 11 cha Sheria ya TCRA, 2003 na hatakuwa na maslahi ya kifedha au mengine yeyote ambayo yanaweza kuleta uwezekano mkubwa wa kuathiri utekelezaji wa kazi zote chini ya Sehemu hii;
(e) Awe na nia ya kutumika kama Mjumbe;
(f) Awe mwenye uwezo wa kuhakikisha kwamba uteuzi wake ni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi na maoni ya watu wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya nchi; na
(g) Awe mwenye uwezo wa kutekeleza majukumu na wajibu kwa ufanisi na uaminifu.
WAJIBU NA MAJUKUMU
(1) Kamati itatenda kazi zake kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa katika kifungu cha
27 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12, 2003 pamoja na majukumu mengine kama yalivyoainishwa katika vifungu vya 5 na 6 vya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na kazi nyingine zilizoainishwa katika Vifungu vya 173 na 174 vya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki (EPOCA) ya 2010. Wajumbe watafanya kazi kwa mujibu wa Kifungu cha 27 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12, 2003 ni kama ifuatavyo:-
(a) Kumshauri Waziri wa Sekta juu ya Sera ya Utangazaji;
(b) Kufuatilia na kudhibiti maudhui ya Utangazaji;
(c) Kushughulikia malalamiko kutoka kwa watoa huduma na watumiaji; na
(d) Kufuatilia maadili ya Utangazaji yanafuatwa/kutekelezwa.
(2) Kamati itafanya kazi nyingine kulingana na Mamlaka itakavyozitoa kwa Kamati.
(3) Kufanya majukumu na kazi nyingine kwa kadri zitakavyoamuliwa na Mamlaka kwa mujibu wa Sheria.
Maombi yawasilishwe kupitia anuani iliyopo hapa chini kabla ya tarehe 13 Machi, 2025.
Imetolewa Tarehe 27 Februari 2025.
Dkt. Jabiri K. Bakari
MKURUGENZI MKUU
Jengo la Mawasiliano, Na. 20 Barabara ya Sam Nujoma, S. L. P 474, 14414 DAR ES SALAAM, TANZANIA.
Simu: +255 22 2199760-9 / +255 22 2412011-2 / +255 784558270-1 Nukushi: +255 22 2412009-10
Barua pepe: [email protected], [email protected], Tovuti: www.tcra.go.tz